WAKUU wa Wilaya (Ma-DC) na Wakurugenzi nchini, ambao hawajakamilisha
kutengeneza madawati, yanayokidhi idadi ya wanafunzi katika shule za
maeneo yao, wamepewa siku 14 kukamilisha kazi hiyo.
Imeelezwa kuwa wanafunzi watakapofungua shule, lazima wakae kwenye madawati hayo.
Wakuu wa wilaya na wakurugenzi, watakaoshindwa kutimiza agizo hilo
hadi ifikapo Desemba 30, mwaka huu, watakuwa wamejifukuzisha kazi
wenyewe.
Aidha, wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kwenda
kidato kwanza mwakani, wanaanza masomo yao kwa awamu moja, badala ya
awamu mbili tofauti.
Agizo hilo lilitolewa jijini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Arumeru katika
ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Aliagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote nchini kuwa hadi Desemba
30, mwaka huu wilaya zote zenye upungufu wa madawati ziwe
zimekamilisha.
“Wale ambao watashindwa kufanya hivyo, watakuwa wamejifukuzisha kazi
wenyewe” alisema. Akizungumzia ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo,
Majaliwa alisema kuwa hadi Desemba 30, mwaka huu, wawe wamefikia
asilimia 50, tofauti na hali ya sasa ambapo wamekusanya asimilia 30 tu.
“Ongezeni kasi ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zenu na
mhakikishe kila mtu anafanya kazi zake kwa kumheshimu mwenzie,” alisema
Waziri Mkuu.
Serikali inahitaji haraka madawati ili kuondoa uhaba unaozikabili
shule za sekondari na msingi wa madawati. Hali halisi ikoje? Hadi sasa,
zaidi ya madawati milioni moja, sawa na asilimia 88 ya madawati
yanayohitajika katika shule za msingi na asilimia 95 kwa shule za
sekondari, yamepatikana. Kwa shule za msingi, imebaki asilimia asilimia
12 kumaliza tatizo la madawati, huku shule za sekondari imebaki asilimia
5.
Mikoa sita ambayo ina hali mbaya na haijatekeleza kikamilifu agizo
hilo la madawati ni Mwanza, Kigoma, Mara, Rukwa, Simiyu, Dodoma na
Geita, ambapo Geita inadaiwa madawati zaidi ya 80,000 ya shule za msingi
na sekondari.
Mwanza inadaiwa madawati 41, 438, Kigoma madawati 31,171, Mara
madawati 16,978, Dodoma madawati 14,873, Rukwa madawati 10,978 pamoja na
Mkoa wa Simiyu.
Mkoa wa Mwanza unaundwa na wilaya za Nyamagana, Ilemela, Misungwi,
Kwimba, Ukerewe, Magu na Sengerema, wakati wilaya za mkoa wa Kigoma ni
Buhigwe, Uvinza, Kakonko, Kasulu, Kibondo na Kigoma.
Wilaya za mkoa wa Mara ni Tarime, Bunda, Butiama, Musoma, Serengeti
na Rorya na Mkoa wa Rukwa una wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Mkoa wa Simiyu wilaya zake ni Bariadi, Maswa, Busega, Meatu, Itilima
na Mkoa wa Dodoma wilaya zake ni Kondoa, Bahi, Mpwapwa, Kongwa, Dodoma,
Chamwino na Chemba, wakati mkoa wa Geita wilaya zake ni Geita, Chato,
Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale.
Mikoa ambayo imemaliza tatizo hilo la madawati kwenye shule za msingi
na sekondari ni 14 ambayo ni Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Arusha,
Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Manyara, Pwani, Shinyanga,
Singida na Tabora.
Mikoa mingine iliyosalia, imebakiza idadi ndogo ya madawati ambayo inakaribia kukamilika. Tanzania Bara ina mikoa 26.
0 maoni: