Thursday

Rais Magufuli amsimamisha kazi Kaimu Katibu wa Tume ya Mipango

Rais John Magufuli amemsimamisha kazi Kaimu Katibu wa Tume ya Mipango (Wizara ya Fedha), Florence Mwanri aliyeidhinisha kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) (Terminal 3) kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ili kupisha uchunguzi.
Rais Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya na kuagiza shughuli za ujenzi wa uwanja huo ziendelee kuanzia leo.
Taarifa iliyotolewa Jumanne hii na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli alisikitishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa, ikiwamo Serikali kukubali gharama kubwa za mradi ambazo ni Shilingi 560 bilioni kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na jengo linalojengwa.
“Hivi kulikuwa na sababu gani za ninyi wataalamu wa serikali kukubali gharama kubwa namna hii, hivi hili jengo linafanana na Shilingi 560 bilioni? alihoji. Halafu mlikuwa na haraka gani kuidhinisha kuanza awamu ya pili ya ujenzi kabla ya kumaliza awamu ya kwanza?” aliendelea kuhoji Rais Magufuli.
Katika ziara aliyoifanya jana ilielezwa kuwa mkandarasi anayejenga uwanja huo, kampuni ya BAM International alitangaza kusitisha ujenzi kuanzia jana kutokana na kutolipwa madai yake. Hata hivyo, Rais Magufuli ameahidi kulipa fedha hizo haraka.
Aidha Rais Magufuli ameviagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi katika mradi huo.

SHARE THIS

0 maoni: