OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeokoa Sh bilioni 4.38 ambazo zingetumika
na watumishi wa Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya safari za
ndani.
Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene
alibainisha hayo katika kipindi maalumu cha Siku 100 za Serikali ya
Awamu ya Tano kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
“Katika kipindi cha siku
95, tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo watumishi wa
halmashauri wangezitumia katika safari za ndani zisizo na tija na
hazijalenga kumkomboa mwananchi huyu ambaye hana dawa na hana barabara,” alisema Simbachawene.
Akizungumzia uwajibikaji wa watumishi
katika halmashauri nchini, Simbachawene alisema ili kuhakikisha
halmashauri hizo zinafanya kazi ipasavyo, wameunda kitengo cha ukaguzi
ambacho kina kazi ya kudhibiti na kufuatilia utendaji wa kazi za
halmashauri.
“Tamisemi tuna deni kubwa,
kwani sisi ndio tunaotegemewa na wizara kutafsiri mipango yao ya elimu
afya, miundombinu na sekta nyingine. Tamisemi ni wakala wa serikali kwa
wananchi,” alisema na kuongeza kuwa watendaji wa
halmashauri ambao hawataki kwenda na kasi ya Rais Magufuli, basi
wataondolewa katika nafasi zao bila kuonewa haya.
“Tutahakikisha
tunawachukulia hatua wezi wote, wabadhirifu na wasio waadilifu, huwezi
utupishe. Tutawapima kwa jinsi wanavyoondoa kero kwa wananchi,”
alisema na kukiri kuwa katika halmashauri kuna matatizo ya uadilifu
jambo linalofanya miradi mingi kushindwa kukamilika na ikikamilika
inakuwa chini ya kiwango.
Aidha, amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanawafikia wananchi na kumaliza kero za wananchi kinyume chake kazi wataiona chungu.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato,
Simbachawene alisema asilimia 95 ya halmashauri zote zimeanza kutumia
mfumo wa elektroniki katika kukusanya mapato na kuwa zile chache ambazo
hazijaanza zimetakiwa kufanya hivyo baada ya kuongezewa muda kidogo.