Tanzania haijapata kushiriki Michuano ya Olimpiki kwa upande wa mpira wa miguu jambo ambalo limeisukuma TFF kuona kuwa ni fursa ya mpira wa miguu kuchezwa hivyo inashirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kufanikisha mipango na taratibu.
Tanzania kwa sasa ina vijana wengi waliotokana na michuano ya Mradi wa kuibua na kukuza vipaji wa Airtel kadhalika na Cocacola ambao wamekuwa chachu ya maendeleo ya timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys.
Vijana hawa wa Airtel, Copa Cocacola na Serengeti Boys wataungana na baadhi ya vijana waliofanya vizuri kwenye Ligi ya Vijana wenye umri wa chini miaka 20 kutoka timu za Ligi Kuu ambao wamezaliwa baada ya tarehe 1 Januari 1997 ili kuunda kikosi imara cha awali kuelekea kufuzu kwa michuano ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan, mwaka 2020.
Kwa kufuata utaratibu wa maandalizi ya Serengeti Boys na kwa kushirikiana na TOC timu hii itapewa mazoezi na michezo ya kujipima nguvu ndani na nje ya nchi.
0 maoni: