Taarifa zilizotufikia zimedai kuwa Roma na watu wengine waliokuwa wameshikiliwa tangu Jumatano hii wamepatikana wakiwa salama.
Mkuu wa polisi (OCD) wilaya ya Kinondoni, Abubakar Kunga
amethibitisha kupatikana kwa wote waliopotea. Lakini kwa sasa amesema
wanafanya nao mahojiano ya kipolisi katika kituo cha Oysterbay lakini
baada ya muda mfupi wataongea na waandishi ili kutoa taarifa kamili.
Kupatikana kwao kumefuatia wito mkubwa uliokuwa ukipaishwa na wasanii wenzake na mashabiki kuhusu kuachiliwa huru.
Awali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishina
Simon Sirro alisema bado walikuwa wakiendelea na upelelezi wa tukio la
kupotea (kutekwa) kwa msanii Roma Mkatoliki na wenzake.
Akiongea na waandishi wa habari mchana huu Polisi Central jijini Dar
es salaam, Kamanda Sirro alisema tukio la utekwaji wa Roma na wenzake ni
aina ya matukio ambayo hutokea mara kwa mara.
“Matukio ya utekaji hayajaanza leo, hili la kina Roma na wenzake ni
tukio kama matukio mengine yaliyokuwa ya ujambazi kwahiyo tupeni muda
tupeleleze, tukifika mahali pazuri tutawaita tuwape taarifa lakini
nimeona mitandao mingi inazungumza, jana nikaona wasanii wamekutana
lakini nikajiuliza hivi yangekuwa haya matukio yanatokea ya uhalifu
yanapotokea watu wanakutana ingekuwaje?,” alisema Sirro.
Aliongeza, “Jamani kazi hii tumepewa kwa mujibu wa Katiba na ni
lazima tutimize wajibu wetu kwa hiyo tupeni muda tutakuwa na majibu
mazuri katika hili,” aliongeza.