Tuesday

Ziara ya Rais Magufuli Kagera: Watatu watumbuliwa

Siku chache zilizopita baada ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kuagiza watumishi wote wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera waliohusika katika ukarabati wa majengo ya shule ya sekondari Omumwani ambayo yalionekana kutoendana na thamani ya fedha zilizotumika wachunguzwe, watumishi watatu wa manispaa hiyo wamesimamishwa kazi.
Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani.
Watumishi hao wamesimamishwa Jumanne hii na Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani, baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya maji iliyomo katika majengo ya shule hiyo. Baada ya uchunguzi huo, Athumani alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chibunu Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika moja kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa shughuli hiyo.
Aidha Athuman alisema aligundua ukarabati uliofanywa ulikuwa chini ya kiwango na hauendani na thamani ya Shilingi milioni 119 zilizotolewa na Serikali. “Kwanini wakurugenzi hampendi kufuatilia miradi iliyo katika maeneo yenu? “Kama mngefuatilia mapema, mngegundua ubadhilifu uliofanyika hapa na kuchukua hatua mapema,” alisema Athumani.
“Kwahiyo, naagiza kuanzia leo Januari 3 (jana), mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba uwasimamishe watumishi wote waliohusika ambao ni Mhandisi Kitengo cha Ujenzi wa Manispaa ya Bukoba, Andondile Mwakitalu, Mhandisi Msaidizi, Costane Felix na fundi Charles Kafum,”.
“Hawa lazima wasimamishwe ili kupisha uchunguzi utakaofanyika kwa ajili ya kulinganisha kazi iliyofanywa na kiasi cha fedha kilichotumika kama vinaendana,” aliongeza.
Kwa upande wake Mhandisi Mwakitalu aliyesimamishwa, alisema majengo hayo yalikuwa katika hali mbaya na kwamba ukarabati wake unahitaji fedha nyingi ili yarudi katika hali yake ya kawaida.

SHARE THIS

0 maoni: