Tuesday

Fedha za posho zipelekwe kwenye miradi – Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Agizo hilo alilitoa Jumanne hii, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Kuanzia sasa marufuku wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwamo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Majaliwa.
Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa Shilingi bilioni 130 zilizokuwa zitumike na halmashauri na manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa katika miradi na shughuli za maendeleo.
“Sasa hivi madiwani hakuna kupewa fedha za miradi ya maendeleo mkononi, bali wawasilishe vipaumbele vya miradi yao ili halmashauri husika isimamie malipo yake kwa ajili ya kuepuka migogoro.Madiwani kama mna kampuni haziruhusiwi kufanya kazi katika halmashauri mlizopo ili kuondoa upatikanaji wa zabuni za upendeleo, kitendo kinachoshusha ufanisi wa kazi.”
Aidha waziri mkuu alizitaka halmashauri zote nchini kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi. “Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ruzuku kwa halmashauri zote nchini kulingana na bajeti itakavyoruhusu, tunataka halmashauri zitekeleze miradi yake ipasavyo.”
Katika hatua nyingine waziri mkuu amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

SHARE THIS

0 maoni: