Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye
amekiri kuwepo kwa udhaifu katika sheria ambazo zinaliongoza Baraza la
Sanaa Taifa (BASATA) lililopewa dhamana ya kusimamia na stawisha
shughuli za sanaa nchini.
Waziri Nape
Waziri Nape amedai kwa sasa baraza hilo linakutana na wasanii wakati
wa kuzifungia kazi zao pale wanapokiuka maadili ya kazi za sanaa.
“BASATA ambalo ndio baraza lipo chini yangu sio rafiki kwa msanii,”
Waziri Nape alikiambia kipindi cha XXL cha Clouds FM. “Msanii anakutana
na BASATA unapotakiwa kufungiwa wimbo wake au anapotakiwa kuonywa kwa
kupewa adhabu. Nataka sheria ilifikishe sehemu BASATA awe walezi wa
msanii. Sasa hivi wakiamua kuwa walezi akina Mngereza na wenzake ni kwa
mapenzi yao. Lakini nataka sheria iwalazishe wao sio polisi, wao ni
wazazi wanaotakiwa kulea na kuendeleza,”
Aliongeza, “Hata Bodi ya filamu wasionekane tu wakati wakufungiana,
waonekane pia wakati msanii anaanza kukua mpaka anafika mbali zaidi. Kwa
hiyo changamoto kubwa kwetu mfumo sio rafiki wa kuifanya sanaa yetu
itoke hapa iende mbele,”
Waziri huyo amesema serikali ikirekebisha sheria za sanaa na kuwa
rafiki kwa watumiaji anaamini sekta ya sanaa inaweza kutoa mchango
mkubwa katika kukuza pato la Taifa.
0 maoni: