Monday

Waziri Mkuu afanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Mount Meru,Akerwa na Msongamano Katika Wodi ya Wazazi

 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alifanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ambako kulikuwa na tuhuma za kuibwa watoto, lakini alishuhudia wazazi watatu wakilala kitanda kimoja. 

Ziara hiyo ilitokana na taarifa alizolalamikiwa na wananchi juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kwamba hospitali hiyo ina matukio ya wizi wa watoto wachanga. 

Hata hivyo, jana baada ya kufika katika hospitali hiyo, Majaliwa alishuhudia msongamano katika wodi ya wazazi na kuagiza kuboreshwa hospitali za pembezoni. 

Majaliwa aliagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanaondoa changamoto za ongezeko la wagonjwa na kuboresha huduma katika hospitali hiyo. 
Akizungumzia sakata ya kupotea kwa watoto katika hospitali ya mkoa alivitaka vyombo husika kuendelea na uchunguzi kwa kuwa suala hilo tayari lipo mikononi mwa vyombo vya dola. 

Wiki mbili zilizopita mzazi, Walda Mussa alisema kuwa alijifungua mtoto katika hospitali hiyo lakini hadi alipotoka hakumpata.
“Nilikuja hapa hospitali Oktoba 4 na Oktoba 7 nikajifungua kwa upasuaji wakamchukua mtoto na kumpeleka chumba cha joto, akaja mume wangu akaenda kumuona mtoto mzima, siku ya pili alienda kumuona mtoto pia akiwa mzima lakini siku ya tatu, tulipokwenda wote mimi na mume wangu tuliambiwa mtoto alifariki na hatujawahi kuona mwili wake,” alisema mwanamke huyo hivi karibuni. 
Mganga Mkuu mfadhiwi wa hospitali ya Mkoa Mount Meru, Dk Jackline Urio alipotakiwa kuelezea sakata hilo, alisema kuwa mtoto huyo baada ya kuzaliwa alifariki dunia na baadaye mwili ulipelekwa chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo.

SHARE THIS

0 maoni: