Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema ataingia Ikulu
baada ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa
serikali ijayo itaongozwa na Chadema.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema mkoani Tabora, mjumbe
huyo alisema ana uhakika wa kuingia Ikulu bila ya umwagaji wa damu.
Baada ya kutoa kauli hiyo alishangiliwa na kuwashukuru wana Tabora na
Watanzania kwa ujumla kwa kura walizompa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Alieleza kuwa mhubiri huyo maarufu barani Afrika anayefanya shughuli
zake nchini Nigeria na ambaye alikuja nchini mara baada ya Uchaguzi Mkuu
uliopita, alimpa angalizo kuwa ili washinde ni lazima wawe wamoja,
washikamane na kuwa majasiri.
“Najua waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu
Joshua ametabiri serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,”
alisema Lowassa.
Ikumbukwe Lowassa alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha
urais mwaka jana na ameshaonyesha nia ya kuingia tena kwenye mpambano
huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
0 maoni: