Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imewavua
madaraka walimu wakuu 15 wa shule za msingi wilayani humo, kwa kosa la
kuandikisha wanafunzi hewa 883 na kuisababishia halmashauri hiyo hasara
ya Sh milioni 3.4.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Msalala, Simon Berege, alisema hatua hiyo imetekelezwa baada ya
kufanya uchunguzi wa kuhakiki wa wanafunzi hao kwa kipindi cha kuanzia
Agosti hadi Oktoba mwaka jana katika shule za msingi.
Berege alisema katika uhakiki wa kwanza uliofanyika Agosti hadi Oktoba, mwaka jana, ilibainika kuwepo kwa wanafunzi hewa 639.
Aliongeza kuwa katika uhakiki mwingine uliofanyika Oktoba mwaka huo
kwa kushirikiana Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) walibainika wanafunzi hewa 244.
Alisema kutokana na tatizo hilo, halmashauri hiyo iliwaita walimu hao
wakuu na kuwataka warudishe fedha hizo na walikubali kuzirudisha fedha
katika Ofisi ya Mkurugenzi kabla ya kuvuliwa madaraka yao rasmi kuanzia
Desemba 7, mwaka huu walipokabidhiwa barua zao.
Mkurugenzi huyo aliwataja waliovuliwa madaraka na shule kwenye mabano
kuwa ni Emmanuel Nkwabi (Mhama) aliyelipa Sh 56,000 Sita Kasangi
(Mwakuzuka) aliyelipa Sh 132,000, Iman Gongo (Nyamigege) amelipa Sh
155,000, Fabian Mchiwa (Mwanyaguli) Sh 21,000 na Omari Masani (Ngaya) Sh
86,000.
Aliwataja wengine kuwa ni Vedastus Masonga (Buganzo) Shilingi
215,5000, Bernard Patroba (Nyamididi) Sh 142,000, Abbas Kirua (Gulla)
aliyelipa Sh 26,000, Elisafi Mshana (Shishinulu) Sh 456,500, George
Mabambi (Mbizi) Shilingi 68,000 na Hussen Said (Bukwangu) Shilingi
56,000.
Wengine ni Anthonia Peter (Chella) Sh 168,000, Godfrey Niwagira
(Buyange) Sh 99,000, Aron Sizya (Kashishi) Sh 198,400 pamoja na Jovinus
Katemi (Nyakadoni) aliyelipa Sh 99,000.
0 maoni: