Rais wa Zambia, Edgar Lungu ameitahadharisha Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari (TPA) kuwa Wazambia hawabanwi na urafiki uliopo kati ya nchi
hizi mbili kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam, bali
wanaendelea kufanya hivyo kutegemeana na ufanisi unaofanywa na mamlaka
hiyo.
Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya vitengo vya bandari hiyo
Jumanne hii, Rais Lungu alisisitiza nchi yake itaendelea kupitisha
mizigo kwenye bandari hiyo kama itaendelea kutoa huduma kwa ufanisi
mkubwa kuliko bandari zingine zilizoko katika ukanda wa kusini mwa
Afrika.
“Mimi na Rais Magufuli tuna urafiki wa karibu, nchi mbili hizi pia
zina urafiki wa muda mrefu, lakini Wazambia hawapitishi mizigo yao
katika bandari hii kwa sababu ya urafiki wetu, bali wanachohitaji ni
urahisi na uharaka wa kutoa na kusafirisha mizigo yao,” alisema Lungu.
“Pia hatuwaungi mkono kibiashara eti kwa sababu tu nchi mbili hizi
tuna uhusiano mzuri, bali tunaangalia ni wapi ambako wanatoa huduma kwa
haraka na kwa ufanisi. Kwani naamini hata tusipowapa biashara undugu
wetu wa damu utaendelea, lakini hatuendi kwingine tunakuja hapa kwa
sababu ya ufanisi,” aliongeza.
Aidha Rais huyo aliitahadharisha mamlaka hiyo kuwa wanatakiwa
kuhakikisha kila siku wanabuni namna ya kuboresha huduma zao kwa kuwa
kuna nchi jirani pia zinatoa huduma kama wanayotoa wao na ambao
wangependa kupata biashara zaidi.
0 maoni: