Seriikali imesema kwamba haitawalipa
watu wote ambao wamebomolewa nyumba zao kwa kujenga mabondeni au kujenga
maeneo ya wazi,hifadhi ya barabara, au maeneo yaliyotengwa kwa shughuli
maalumu.
Hayo yameelezwa Bungeni na Naibu Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Angelina Mabula wakati
akijibu swali la Mbunge wa Wingwi Kisiwani Zanzibar Juma Kombo Hamad
ambaye ametaka kujua ni lini serikali itawalipa fidia wananchi ambao
wamevunjiwa nyumba zao bila ya serikali kuwalipa kwani wakati wakijenga
serikali iliwaona na kukaa kimya.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Mabula
amesema kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na sheria ya
mipango miji ya mwaka 2007 inaweka bayana sehemu ambazo wananchi
hawatakiwi kujenga ikiwemo maeneo oevu, mabondeni, na vyanzo vya maji
ambapo mwananchi akitaka kujenga ni lazima ajenge umbali wa mita 60
maeneo hayo.
Bi. Mabula ameongeza kuwa kutokana na
wananchi kukiuka maagizo hayo serikali haitawalipa fidia hivyo ni wajibu
wa wananchi kufuata sheria za nchi ili kuepuka migongano isiyo ya
lazima.
Aidha Bi. Mabula amezitaka halmashauri
zote nchini kuwa makini katika kusimamia sheria kwani imebainika kuwa
nyumba nyingi huwekwa alama ya X na halmashauri lakini ufuatiliaji
unakuwa haupo ndiyo maana matatizo hayo yamekuwa yakijirudia.
0 maoni: