Tuesday

Waziri mkuu awakalisha kiti moto watumishi wa Ngorongoro kwa tuhuma za kuiba faru

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa amefichua uhalifu uliofanywa na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wa hifadhi za taifa, ambao walihongwa Sh milioni 100 na kushiriki kumwiba faru maarufu aliyepewa jina la John kutoka hifadhi hiyo.
waziri-mkuu-kassim-majaliwa 
Huku akitaja majina ya wahusika wa uhalifu huo, ameagiza ifikapo kesho, apewe maelezo ya nini kilichotokea kwa mnyama huyo adimu ambaye kwa taarifa alizonazo amekufa akiwa Hifadhi ya Serengeti eneo la Grumeti mkoani Mara.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana katika ofisi za makao makuu ya mamlaka hiyo wakati akizungumza na watumishi pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafugaji ambapo ilikuwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.
Wakati akiendelea na hotuba yake, ghafla alimsimamisha mmoja wa mtumishi wa NCAA, Cuthbert Lemanya ambaye ni Mkuu wa Kanda katika eneo la Kreta na kumuuliza “Faru John yuko wapi?” Kabla ya kupewa jibu, Waziri Mkuu akawasimamisha watumishi wengine wawili ambao ni Israel Noman, Patrice Mattey na kuwauliza, “Faru John yuko wapi? Yupo Kreta? “Nina taarifa zenu kuwa mliiba faru John Kreta na kumpeleka VIP Grumeti Serengeti, Desemba 17, mwaka jana ambapo mliahidiwa shilingi milioni mia mbili, na badala yake mkapewa shilingi milioni mia moja.Na mmepata mgawo wa shilingi milioni mia moja halafu mnataka kusingizia kuwa amekufa, yupo wapi Faru John,” aliuliza tena Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu alisema watumishi wengine waliohusika ni Meneja Utalii aliyemtaja kwa jina moja la Kileo ambaye awali aliletwa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuja NCAA kwa ajili ya kusaidiana na wenzake kuiba faru John na baada ya hapo alihamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Pia alimtaja mhifadhi mwingine kwa jina moja la Macha ambaye awali alikuwa hifadhi ya Mkomazi.
“Ninaagiza Kileo na Macha kwa pamoja warudishwe hapa mara moja waje kujibu Faru John yuko wapi,” alihoji Waziri Mkuu na kuongeza kuwa Faru John aliyeondolewa NCAA taarifa alizonazo sasa amekufa, hivyo anataka nyaraka zote zilizotumika kumuondoa NCAA vikiwamo barua za kila vikao vilivyokaa.
Pia ameagiza taarifa ya daktari aliyethibitisha kufa kwa faru huyo huyo pamoja na kuagiza pembe zake kufikishwa kwake.
“Ninataka taarifa zote za faru huyo, barua za vikao vilivyokaa kuamua Faru John aondoke, pia nataka pembe zake na taarifa ya daktari aliyeithibitisha kufa kwa faru huyo,” alieleza Waziri Mkuu na kuongeza: “Halafu Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe hata wewe walikudanganya, hukuwa unajua faru huyu alivyoondoka. Nahitaji taarifa hizi kabla ya Desemba 8, mwaka huu.”
Alimuagiza Mhifadhi Mkuu wa NCAA kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu, Sezzary Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha; na sasa anahojiwa na Takukuru.
“Kuanzia leo Mkurugenzi Mkuu wa NCAA nakuagiza usimamishe kazi hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Haiwezekani mtumishi awe anachunguzwa na Takukuru halafu aendelee kuwa ofisini atavuruga uchunguzi asimamishwe hadi taratibu zote zimalizike,” alieleza Waziri Mkuu.
Aidha, alimhoji Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Fred Manongi kueleza zilipo Sh bilioni moja alizotoa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete za kujenga ranchi kwa ajili ya wafugaji wa Tarafa ya Ngorongoro.
Akijibu swali hilo, Manongi alisema wakati rais anatoa fedha alikuwa hajateuliwa kuwa Mhifadhi Mkuu wa NCAA. Baada ya majibu hayo, Waziri Mkuu alimuagiza Manongi kufanya uchunguzi juu ya fedha hizo na kusema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ililalamikiwa sana na wadau wa utalii na ina madudu mengi na watu wanafanya NCAA kama shamba la bibi.
Source: Habari Leo.


SHARE THIS

0 maoni: