Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
amesema walimu wa Sayansi watakaoajiriwa na serikali, watalazimika
kutuma vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Profesa Ndalichako, wakati akifungua mkutano
mkuu wa mwaka wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania (Tahossa). Pamoja
na kuzungumzia mabadiliko hayo katika mfumo wa ajira, alisema nia ya
serikali kuimarisha elimu ya sekondari, ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ufundishaji wa masomo hayo ya Sayansi.
Aidha alisema walimu wakuu wana wajibu wa kuwa wasimamizi na wakaguzi
wa kwanza wa wanafunzi ili kuiboresha elimu ya Tanzania, wakizingatia
kuwa elimu ya sekondari ni kiungo muhimu katika kuendeleza elimu nchini.
Vile vile, aliwataka wakuu hao kupeleka takwimu sahihi za wanafunzi
waliopo katika shule zao ili kuisaidia serikali katika kupanga bajeti
ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe wakati mwingine huwa najifanyisha nimepoteza
takwimu ya shule fulani nikitumiwa inakuwa tofauti na ile ya mwanzo,
niwaombe walimu mkalisimamie hili ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti
yenye tija,” alisema.
Kwa upande wake Rais wa Tahossa, Bonus Nyimbo wakati akisoma risala
aliiomba serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa
wanafunzi shuleni, kwani imekuwa ikichangia kushusha ufaulu wa baadhi ya
wanafunzi.
0 maoni: