Trump amshinda Clinton majimbo muhimu Marekani
Wagombea urais wawili wakuu wa urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump wanakaribiana sana katika matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.
Lakini mgombea wa Republican Bw Trump ameshinda majimbo mengi ya kusini mwa Marekani naye Bi Clinton akashinda majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la ABC News.
Chama cha Republican kinaonekana kuwa njiani kuhifadhi wingi wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.
Kama ilivyotarajiwa, Bw Trump ameshinda katika ngome za Republican katika majimbo ya Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana, West Virginia, Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas, ABC News wanakadiria.
Bw Trump pia anakadiriwa kushinda Arkansas, Kansas, North Dakota, South Dakota, Montana na Wyoming.
Shirika hilo linakadiria Bi Clinton atashinda ngome za Democratic majimbo ya New York, New Jersey, Connecticut, Massachusetts, Maryland, Vermont, Delaware, Illinois, Rhode Island na District of Columbia.
Mshindi anahitaji kupata kura 270 kati ya jumla ya kura 538 za wajumbe ndipo atangazwe mshindi.
0 maoni: