Wananchi hao, walitoa kilio chao hicho mbele ya Makonda, alipowatembelea katika eneo la Keko ili kusikiliza kero zao.
Wakitoa dukuku zao, wananchi hao walisema wamechoshwa na unyanyasaji wa jeshi hilo kwani, baadhi ya askari wasiyo waaminifu wilayani humo wamekuwa wakiendekeza rushwa, unyanyasaji, kuwabambikia kesi na kamatakamata raia wasiyo na hatia.
Fatuma Said, alilalamika kuwa, hivi karibuni kijana wake ambaye ni mwendesha pikipiki bodaboda, alikamatwa na polisi na pikipiki yake kupelekwa kituo cha kati, ambako kijana huyo alitozwa sh. 200,000.
“Pamoja na kutoa fedha hizo kijana wangu hakupewa pikipiki, nilipofuatilia niliambiwa nipeleke sh.400,000 na kadi, nikapeleka lakini sikupewa pikipiki hadi leo hii.Hii ni haki,?” alihoji Fatuma.
Alisema anahitaji kujua haki yake na haki za bodaboda wengine ambao wamekuwa wakinyanyaswa na kutozwa fedha bila utaratibu.
Mkazi mwingine wa eneo hilo ambaye hakutaja jina lake, alisema, kumekuwa na vitendo vya unyanyasaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya askari polisi katika eneo hilo, ambao hukamata raia wengi wasiyo na hatia kisha kuwapeleka katika vituo vya polisi na kuwataka watoe fedha ili waachiwe.
“Mkuu wa mkoa tunaomba uchunguze hili. Tunanyanyswa sana. Tunakamatwa bila hatia. Vituo vya polisi Chang’ombe, Makangarawe na Kilwa vimekithiri kwa rushwa na unyanyasaji wa raia.Chunguza utabaini ukweli,”alisema kijana huyo akidai amekamatwa mara kadhaa bila hatia na polisi.
Kufuatia tuhuma hizo, Makonda alimtaka Kamanda wa Polisi Mkoa Maalum wa Temeke, Gires Muloto, kutoa majibu juu ya tuhuma hizo, ambapo Muloto alisema atashughulikia kikamilifu askari wite wanaokwenda kinyume na sheria ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji.
“Nileteeni majina yao ili tuwashughulikie. Ukiona askari anatataka kukutoza faini isiyostahili au rushwa basi mlete kwangu ili tumshughulikie. Tutamfukuza kazi na kumchukulia hatua za kisheria,”alisema Muloto.
Kufuatia madai hayo, Mkuu wa Operesheni Maalum mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondwa, ameagiza wananchi kumpelekea majina ya polisi wote wasiyo waaminifu wanaoendekeza vitendo vya rushwa na kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha kamanda Mkondwa, alimtaka Fatuma Saidi aliyelalamika kuhusu kutozwa sh.6,000,000 na polisi wa kituo cha kati kama faini ya pikipiki yake kuonana naye jana hiyohiyo ili askari mhusika aweze kusakwa na kuadhibiwa.
Mkondya aliahidi kuwa, ikiwa askari huyo atapatikana na kuthibitika alichukua fedha hizo na kama kweli pikipiki ni halali basi atamfukuza kazi mara moja kisha kumshitaki katika mahakama ya kijeshi.
“Nikabidhiwe jina la huyo askari ambaye alichukua sh.6,000,000 na pikipiki yake kama ni halali basi ataipata leoleo. Askari huyo tutamshitaki mashtaka ya kijeshi na kama kweli amechukua fedha hiyo atafukuzwa kazi maramoja,”alisema Kamanda Mkondya.
Kwa upande wa Makonda, alionya vikali juu ya askari wote wanaojihusisha na vitendo va unyanyasaji kwa raia rushwa na kuwataka wananchi kuanza kutumia teknolojia ya simu kuwarekodi kisha kuwaripoti katika mamlaka husika.
“Watengenezeeni mtego ikiwa ni pamoja na kuwarekodi kwa simu kisha mtuletee ili tuweze kuwashughulikia,”alisema Makonda.
Katika hatua nyingine, Makonda amemuagiza MKurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Temeke, kulitafutia ufumbuzi haraka suala la kuzibwa kwa njia na Kampuni ya Oil Com na Mona Lissa Feniture, ambapo wananchi wamelalamikia kampuni hizo kujenga ukuta na kuziba njia za asili licha ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoa maagizo ya kuvunjwa kwa ukuta huo.
0 maoni: