BUNGE LASIMAMISHWA KWA MBINDE KISA KIFO CHA SITA
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu amekumbana na kibano cha wabune baada ya wawakilishi hao wa wananchi kuzua zogo wakilazimisha shughuli za kikao cha sita ziahirishwe kuenzi kifo cha Spika mstaafu, Samuel Sitta.
Sitta aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tisa na pia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alifariki dunia nchini Ujerumani.
Tafrani hiyo imeanza baada ya kuwatambulisha wageni waliofika bungeni ambapo Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Munde Tambwe alisimama na kuomba mwongozo kwa Spika.
Amesema kutokana na taarifa za msiba wa Sitta, Taifa na hususani wakazi wa Tabora wamepoteza kiongozi mahiri.
“Sitta alikuwa mbunge wa muda mrefu alikuwa Spika wa Bungekwa muda mrefu na pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba la Kihistoria,” amesema akimwaga machozi huku akikatiza mazungumzo.
“Kwa niaba ya wabunge wenzangu, naomba Bunge liahirishwe ili kupata muda wa kuomboleza na kutafakari,” amesema.
Ombo hilo liliungwa mkono na Mbunge wa Manyoni Magharibi (CCM), Elibariki Kingu kwa kumfuata Munde kwenye kiti chake na kumbembeleza.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, amesema licha ya kwamba anakubaliana na mbunge huyo kuwa msiba ni mkubwa na umeligusa Taifa na kwamba ofisi ya Bunge ilimhudumia kwa matibabu, Bunge linaendeshwa kwa kanuni.
“Kanuni zinasema anapofariki mbunge. Mheshimiwa Spika alishastaafu kuwa mbunge, naomba tuendelee hadi hapo kutakapokuwa na maelekezo mengine,” amesema Zungu.
Kauli ya Zungu ilimnyanyua Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kwa kutumia Kanuni ya Bunge ya 152 ambayo aliinukuu, “Endapo mbunge atafariki wakati bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya kuomboleza.
“Toka nchi yetu ipate uhuru tulikuwa na maspika kadhaa, maspika wote waliopoteza maisha baada ya kustaafu, Bunge halikuwa kwenye vikao vyake.
“Walipofariki dunia Adam Sapi na Elasto Mang’enya Bunge halikuwa kwenye session (vikao), hivyo leo imetokea tupo kwenye vikao, tunaweza kutumia nafasi hii kwa heshima ya Samuel Sitta,” amesema.
Pia, Zitto amesema Bunge haliendeshwi kwa kanuni peke yake, bali linaendeshwa kwa desturi na kwa maamuzi ya maspika na hivyo anaweza kufanya maamuzi yatakayosaidia baadaye endapo ikitokea hali kama hiyo.
“Naomba kutoa hoja Bunge liahirishe shughuli zake leo (jana) kwa ajili ya kumuenzi Spika Mstaafu Samuel Sitta ambaye ameitumikia nchi kwa muda mrefu sana,” amesema Zitto.
Hata hivyo, Zungu akasisitiza maamuzi yake yanabaki kama aliyoyatoa awali, msimamo ulioibua kelele kutoka kwa wabunge wote ndani ya Bunge na hivyo kupoteza hali ya utulivu.
Baada ya kushindwa kurejesha utulivu, Zungu akasema kwa mujibu wa uzito wa suala lenyewe Kamati ya Uongozi wa Bunge ikutane kwa dakika 15 huku Bunge likiendelea na shughuli zake.
Akasema baada ya kikao hicho cha muda mfupi watatoa majibu ya kile kilichoamuliwa lakini kelele za wabunge ziliendelea.
Baada ya hali hiyo, Zungu akalazimika kusitisha kwa muda wa dakika 15 ili kusubiri majibu ya kikao cha Kamati ya Uongozi.
Baada ya kikao hicho, Zungu akasema kamati hiyo imeridhia Bunge liahirishwe hadi leo saa tatu asubuhi
0 maoni: