Monday

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kasulu Mjini(NCCR) na kuhamia ACT-Wazalendo, Moses Machali ahamia CCM

 
 
Kutoka mezani kwangu Moses Joseph Machali, Tarehe: 21/11/2016

Napenda kuutaarifu umma wa Watanzania kupitia kwenu waandishi wa habari kwamba ni jambo la ajabu na aibu kwa watu makini na wenye kuhitaji mabadiliko ya kweli Kuacha kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini Uongozi wa Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli bila kusahau utendaji makini wa Waziri Mkuu wake Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa (Mb) pamoja na mawaziri mbalimbali wameonesha kutaka kufuata mwenendo wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake.

Mimi Moses Joseph Machali niliyefanya sana siasa za Upinzani hapa nchini na niliyepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala nchi hii; niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa nguvu na uwezo wangu wote nikishirikiana na wapinzani wenzangu, ninaamua kujiunga na watu wanaonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi yetu Tanzania. Watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi yetu kwa maendeleo enedelevu ni jamii ya akina Magufuli, Kasim Majaliwa, nk.

Mwaka mmoja wa Uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi wake kupitia hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya ufisadi uliokuwa umeigubika nchi yetu, inatosha kabisa kwa mtu yeyote makini kufanya uamuzi wa kumuunga mkono au kutokumuunga mkono Rais Magufuli.

Mimi nimechagua kumuunga Mkono Rais kwa vitendo, kwa sababu ninaposoma Rekodi yangu ya enzi nikiwa Mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge ni kwamba nilipinga mnoo wizi na ufisadi wa kila aina; Nilipinga Matumizi ya fedha serikalini yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa (Rejeeni hotuba yangu ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, nikiwa Waziri Kivuli wa wizara hiyo ya mwaka 2014/2015 na 2015/2016), vilevile bila kusahau hotuba zangu mbalimbali Bungeni na nje ya Bunge.

Kwa kushirikiana na wapinzania wenzangu enzi hizo tulishauri na kupinga ufisadi wa kila aina, tuliitaka serikali kufanya mambo yenye tija kwa taifa na sasa kila mwenye macho anaona hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano. Miradi kama ya Ujenzi wa Reli, Ununuzi wa ndege mbili na mipango ya kununua ndege zaidi kama namna ya kulifufua shirikia la ATCL ni mambo tuliyoyahitaji kuyaona wapinzani; sasa yanafanyika. Wale wenye dhamira ya dhati ya kuona nchi yetu ikipiga hatua, kamwe hatuwezi kubeza mambo hayo bali kuyaunga mkono.

Wale tuliosema na kupiga kelele kwamba Serikali ni dhaifu ktk kuwachukulia hatua watu mbalimbali wenye dhamana serikalini walioonekana kufanya vibaya serikalini ktk nafasi zao, leo tunaona kumekuwepo na kasi nzuri ktk kuwachukulia hatua watu hao. Hata hivyo leo hii upinzani umepiteza mwelekeo kwa sababu unapingana na kile ulichokihubiri nchini.

Agenda ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena bali ya JPM na CCM yake au yao. Wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia na kuyahubiri huko nyuma. Hakika huo siyo uungwana bali aina mpya ya ufisadi nchini na usaliti kwa agenda zao.

Kama kweli sisi tumeokuwa wapinzani na tulioonesha kupinga kwa nguvu zote ufisadi ulioiumiza nchi hii tulimaanisha yale tuliyoyahubiri na kuwaaminisha watu basi tunao wajibu wa kuacha tabia ya kuwa vigeugeu kwa mambo tuliyoyaamini na kuyahubiri. Kutofanya hivyo basi ni mwendelezo wa ufisadi kwa maslahi binafsi.

Ni nani asiyeona kwamba serikali ya awamu ya tano inafanyia kazi mambo mengi tuliyoyapigia kelele? Au tunajifanya kutokukubali ukweli unaoishi kwa ule msingi wa upinzani wa Tanzania kwamba Tukimuunga mkono Mtawala kamwe hatutapata kuaminiwa na wapiga kura nchini na hivyo tupinge tu hata kama ni ukweli? Nadhani kinachofanyika ni mwendelezo wa kupinga hata mazuri ili kutafuta fursa ya wapinzani kukubalika kisiasa zaidi hata kwa njia na mbinu haramu kama kawaida ya siasa zilizo zoeleka hapa nchini kwa miaka mingi.

Taifa hili haliwezi kuendelea kwa kuwa na siasa za kutokukubaliana na ukweli unaoishi. Kama dhamira ya kila mtanzania ikiwemo wapinzani ni kuona nchi ina move basi hatuhitaji kuwa watu wa kupingapinga hata yaliyo mema bali kuyaunga mkono yale yaliyo mema bila kujali yanafanywa na nani bali msingi mzuri unapaswa kuwa ukweli kwa kila jambo.

Serikali ya awamu ya tano imeonesha njia ktk mambo mengi na inastahili kuungwa mkono. Safari ni hatua na ninaamini kwamba hata yale yanayoonekana kutokufanyiwa kazi ndani ya mwaka mmoja uliopita na ambayo yalishindikana huko nyuma, bado yanaweza kuja kufanyiwa kazi huko mbeleni. Serikali ya JPM imejitahidi sana tukilinganisha na huko tuliko toka. Uongozi huu unafanana sana na ule wa akina Hayati EDAWARD MORINGE SOKOINE chini ya hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere.

Daima ninaamini ktk yale ninayoyaamini pasipo kufungwa na ukada bali kuangalia ukweli ni upi. Hata kelele wanazopiga baadhi ya watu kwamba maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya Magufuli ni propaganda tu kwa sababu hakuna uhusiano wa maisha magumu na suala la KUDHIBITI wapiga dili wa fedha na mali za umma bali tukubali kwamba wapiga dili waliozoea kupiga dili na kuziingiza fedha walizopiga ktk mzunguko kwamba siyo jambo la msingi ktk kujenga uchumi imara.

Uchumi imara hauwezi kujengwa kwa kuruhusu ubadhirifu wa fedha na mali za umma au hata za mtu mmoja mmoja. Kinachoonekana hivi sasa ni kama nchi inasukwa upya na hivyo tuwaunge mkono viongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa mema wanayoyafanya na kuwashauri kurekebisha ktk yale ambayo hayajakaa vizuri. Tuachane na siasa nyepesi za kutaka kuona kwamba mazuri ni yale yanayofanywa na wapinzani huku mambo hayohayo yakifanywa na CCM yaonekane hayafai na kutajwa kuwa ni ya hovyo. CCM ya JPM siyo ile ya 2015 kurudi nyuma kidogo. Hii ni tofauti na ninaiunga mkono.

Hivyo basi leo Tarehe 21/11/2016 ninatangaza rasmi kwamba ninajiunga na timu JPM kwa maslahi ya taifa kwa kuwa sioni sababu ya kupingana na yale niliyoyapigania na itakuwa ni sawa na mtu kupigana na kivuli chake mwenyewe. Kwaherini Upinzani nimeamua kuanza siasa mpya za masuala yale niliyoyaamini na ninayoyaamini. Imani ni Matendo Na Matendo ni imani. Piga vita ufisadi kwa imani na Matendo.

Moses Joseph Machali
X-mbunge, Kasulu Mjini 2010-2015,

SHARE THIS

0 maoni: