Saturday

Spika ana mamlaka kisheria ya kuomba vyombo vya dola kumsaidia kumkamata mtu – Mdee

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amesema Spika ana mamlaka ya kisheria ya kuomba vyombo vingine vya dola kumsaidia kumkamata mtu huku akisema kuwa ameamua kuwahi Dodoma kuepuka kukomolewa na Spika Ndugai aliyeagiza afike mbele ya Kamati ya Maadili jana asubuhi na kuagiza polisi wamsake popote alipo, ikiwezekana apelekwe akiwa amefungwa pingu.
Mdee, ambaye alikuwa Dar es Salaam wakati amri hiyo ikitolewa juzi saa 5:00 asubuhi, aliwasili Dodoma jana, lakini suala lake litajadiliwa leo. “Spika ana mamlaka ya kisheria ya kuomba vyombo vingine vya dola kumsaidia kumkamata mtu,” alisema Mdee alipoongea na gazeti la Mwananchi.
“Kwa sababu hiyo, ana uwezo wa kutumia mamlaka hayo kumkomoa mtu. Ndiyo maana nikaja mwenyewe Dodoma. Niliacha majukumu mazito niliyokuwa nayo ili lengo lake la kunikomesha lisifanikiwe,” aliongeza. Spika Ndugai, aliyezungumza kwa ukali, alisema anajua kuwa Mdee alikuwa nje ya Dodoma, lakini akataka awe amefika mbele ya kamati hiyo jana muda sawa na ule aliokuwa akitoa maagizo hayo juzi.
Mdee anatuhumiwa kutoa lugha mbaya kwa Spika, Rais na wabunge wakati wa mjadala uliokuwa mkali wa nafasi za wagombea wa Chadema na CUF katika Bunge la Afrika Mashariki.
Mdee pamoja na Kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kufika watahojiwa na kamati hiyo leo.

SHARE THIS

0 maoni: